SHIZA KICHUYA:
Shujaa wa Simba anayewakosesha usingizi mabeki, Ligi Kuu Bara (VPL).
Kasi yake Uwanjani yafananishwa na mabasi ya 'Mwendokasi'
NA ABDUL DUNIA
Agosti 20 mwaka huu, pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) lilifunguliwa na klabu 16 zilishuka kuanza kuchuana kuwania ufalme wa soka nchini Tanzania Bara msimu huu.
Ligi hiyo ilianza kwa ushindani wa aina yake huku tukiishuhudia timu ya Mbao FC ya Mwanza ikifanya kweli baada ya kupanda daraja kwa bahati.
Ndio ilipanda kwa bahati baada ya TFF, kuzishusha daraja timu za Geita gold mine, JKT Kanembwe na Polisi Tabora kutokana na tuhuma za upangaji wa matokeo kwenye michezo ya mwisho.
Wakati Ligi hiyo ikiendelea kutimua vumbi huku Simba ikiwa inaongoza kwa alama 20 nyuma ya Stend United yenye alama 16 kumekuwa na matukio mbalimbali ya kufurahisha na kustaajabisha miongoni mwa wachezaji wanaoshiriki kwenye ligi hiyo wakiwa na timu zao.
Japo kuwa ni mchezo wa nane wa mzunguko wa kwanza wa Ligi hiyo lakini kuna walioweza kufanya vizuri na wapo walionesha kuwa wamechemsha.
Kichuya amekuwa homa ya jiji huku akiendelea kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na kasi yake na maamuzi ya haraka wakati akiwa uwanjani.
Hakuna shabiki wa Soka nchini Tanzania ambaye halifahamu jina la Kichuya. Hiyo yote ni kutokana na ubora wake wa kusakata kabumbu aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
Mchezaji huyo Mzawa, ameweza kuwafumba midomo mashabiki wengi wa soka waliokuwa wakimbeza kuwa hana kiwango cha kuchezea Simba.
Kichuya amechangia Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa na utamu wa aina yake kutokana na kiwango chake alichokionesha kwenye michezo iliyopita.
Kichuya ameendeleza kuwaonesha watu ubora wake kwenye michezo ya Ligi Kuu ukiwemo mchezo wa Simba dhidi ya Yanga, uliofanyika uwanja wa Taifa Oktoba Mosi mwaka huu.
Ushujaa wake kwenye pambano hilo, uliweza kuwap[oteza wachezaji nyota waliosajiliwa kwa pesa nyingi na klabu hiyo.
Usajili wa nyota Kichuya haukuwa na mbwembwe kulinganisha na wenzake kama akina Laudit Mavugo, Fredirick Blagnon na wengine, lakini kadri ya Siku zinavyosonga anazidi kuwa mwiba kwenye Ligi hiyo.
Kwenye makala haya Uhuru linatazama safari ya Kichuya kutoka kuwa mchezaji wa kawaida hadi shujaa huku jina lake likiwafunika hata mastaa wa VPL kama akina Donald Ngoma, Amis Tambwe, Ibrahimu Ajib, Laudit Mavugo na wengineo.
Kichuya ni nani?
Anaitwa Ramadhani Shiza Kichuya ni mmoja kati ya mawinga wachache mafundi wa kutumia mguu wa kushoto ambaye anatikisa soka la Tanzania kwa sasa kutokana na kipaji chake cha hali ya juu cha upigaji krosi, chenga za maudhi na mtaalamu wa kupiga pasi za mwisho.
Vile vile Kichuya ni mtaalamu wa kucheka na nyavu na hana masihara kabisa anapobaki na goli kipa. Hadi sasa winga huyo ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na mabao 9.
Jina la Kichuya halikuwa maarufu kabla ya michuano ya Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu yaliyofanyika Zanzibar.
Kiwango chake katika michuano hiyo akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa kizuri na ndicho kilichompandisha na kumfanya kuwa gumzo nchini.
Hata hivyo wakati akiwa na Mtibwa mashabiki wa soka Tanzania hawakumchukulia mchezaji huyo kama tunu ya Taifa kama wanavyomuona msimu huu.
Katika michuano hiyo ya Mapinduzi, Kichuya alifanya mambo makubwa kutokana na uwezo wake uwanjani kiasi cha kuzivutia klabu za Simba, Yanga na Azam ambazo zilianza kupigana vikumbo kusaka saini yake kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao.
Atua Simba, Akabidhiwa Okwi
Vita ya kusaka saini yake ilimalizwa ambapo Simba ilifanikiwa kuibuka mshindi baada ya kumsajili na kumpiga kitanzi cha miaka miwili ambapoa mkataba wake ulidaiwa kuwa na thamani ya dau la Shilingi milioni 20.
Muda mfupi baada ya kusajiliwa na Wekundu hao wa Msimbazi, Kichuya alikabidhiwa jezi namba 25 iliyokuwa ikivaliwa na Fundi wa Soka klabuni hapo, Mganda Emanuel Okwi.
Ikumbukwe kuwa Jezi namba 25 ambayo inaheshimika sana Msimbazi kutokana na kuwahi kuvaliwa na nguli wa zamani wa timu hiyo, Mganda Emmanuel Okwi.
Jezi hiyo iliwahi kusababisha mashabiki wa Simba kufurahi kupita kiasi huku wa Yanga wakihuzunika na wengine kuzimia kwa uchungu baada ya kichapo cha mabao 5-0 kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mashabiki wa Simba walishangazwa na viongozi wao baada ya Jezi hiyo kukabidhiwa Kichuya kwa kuwa Okwi alishaondoka klabuni hapo.
Mashabiki hao walianza kuhoji kuwa iwapo Kichuya ataweza kuitendea haki. Lakini mechi saba tu za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ziliweza kuamua kila kitu.
Kila mtu sasa anakubali kuwa staa huyo anastahili kuvaa jezi hiyo.
Amjibu Kaburu
Kichuya alipokuwa anakabidhiwa Jezi hiyo, Makamu wa Rais wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu', alimsistiza kuitendea haki jezi hiyo kwa kuwa inaheshimika sana na mashabiki wa Simba.
Hadi kufikia sasa inaonekana kwa kiasi kikubwa kuwa Kichuya ameamua kujibu maneno ya Kaburu kwa vitendo kutokana na kiwango chake bora alichokionyesha akiwa na jezi hiyo.
Sio mwenzetu
Mechi saba alizoichezea Simba kwenye Ligi Kuu Bara na kuifungia mabao matano zimetosha kubadilisha mfumo wa maisha yake.
Ndio, Sio mwenzetu, kutokana na kuishi kifalme katika timu hiyo.
'Msema ukweli ni mpenzi wa Mungu' msemo huo unaakisi ya kuwa kipindi hiki Kichuya ndiye Mfalme wa Simba.
Kutokana na juhudi zake binafsi uwanjani huku akiwa na chachu kubwa ya kufika mbali kutokana na kipaji alichonacho mashabiki pamoja na viongozi wa Simba wameonekana kumuunga mkono.
Amepania makubwa
Pamoja na mafanikio machache aliyonayoyapata Kichuya anasema kuwa anajiona kama ni mtu mwenye bahati kutokana na nyota yake kung'ara katika kipindi kifupi akiwa na Simba huku akiendelea kutabiriwa kufanya vizuri nje ya nchi.
Kutokana na hali hiyo anasema pia yupo tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali atakazokutana nazo ikiwemo ile ya kuzomewa na mashabiki uwanjani pindi inapotokea anacheza vibaya.
Kujituma ndio Msingi wake
Kichuya anasema mafanikio yake yanatokana kujituma wakati akiwa mazoezini huku akitumia muda mwingi kumsikiliza mwalimu wake Joseph Omog.
Kichuya anafunguka kuwa kila siku huwa anahitaji marafiki wanaompa ushauri mzuri ili aweze kutimiza malengo yake.
Kichuya anasema kuwa anatumia muda mwingi kumuabudu Mungu na kufanya mazoezi kwa bidii ili kutimiza malengo aliyoweza kujiwekea.
Afananishwa na mabasi ya 'Mwendo kasi'
Kutokana na kiwango chake Shiza Kichuya amepachikwa jina la 'Mwendo kasi' na mashabiki zake baada ya kuonesha uwezo wa hali ya juu.
Amefananishwa na mabasi hayo yaendayo haraka kutokana na kasi yake anapokuwa uwanjani huku akiwasumbua mabeki wa Ligi Kuu Bara.
Aiteka Morogoro
Kichuya ndio mfalme wa sasa Mkoani Morogoro kutokana na kiwango chake huku akiwapa raha mashabiki zake kwa bao tamu alilolifunga kwenye mchezo dhidi ya Yanga.
Kichuya ameyafanya majina ya mwanamuziki Afande Sele na bondia Francis Cheka kupotea kwenye ramani ya mkoa huo kutokana na kiwango chake kuimarika siku hadi siku na kuzidi kuwapa raha mashabiki wa Morogoro.
EmoticonEmoticon