TIMU 16 za Ligi Kuu, zitumie Dirisha Dogo kutatua mapungufu yao kwa kina
NA ABDUL DUNIA
LIGI Kuu Tanzania Bara mzunguko wa kwanza umemalizika alhamisi iliyopita kwa Yanga kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1 na kufanya iipumulie Simba kileleni, kwa tofauti ya pointi mbili tu.
Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 33 wakati Simba ikiwa na pointi 35.
Simba imepumuliwa na Yanga kwa tofauti ya pointi mbili kutokana na kupoteza michezo miwili mfululizo, na African Lyon waliochapwa 1-0 pia na Tanzania Prisons waliopigwa mabao 2-1.
Sihitaji kuzielezea kwa undani klabu hizo zenye maskani yake Kariakoo jijini Dar es Salaam, wakati Simba ikiwa maskani yake pale Mtaa wa Msimbazi na Yanga wakiwa pale Jangwani kunapotokea mafuriko mara kwa mara.
Ngoja nisogee kwenye hoja yangu husika, kuwa ni muda muafaka kwa timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kujipanga na kutumia vema nafasi ya usajili wa dirisha dogo ili kujiweka sawa kwa ajili ya mzunguko wa pili.
Dirisha dogo la usajili linafunguliwa Keshokutwa ili kusajili wachezaji kulingana na mahitaji hivyo kutoa mchango mkubwa kwenye timu zao.
Kwa kawaida Soka letu, huwa hesabu kubwa ni mzunguko wa kwanza lakini ikifika mzunguko wa pili kila timu inafanya mambo yake.
Kuna timu ambazo zinapigania ubingwa kweli, wakati kundi la pili ni lile ambalo zipo zipo tu, hazitaki ubingwa wala kushuka daraja, kundi hili ni lile la katikati wakati kundi la mwisho ambalo hili linakuwa linapigana kujinasua kushuka daraja tu.
Tukianza na timu ambazo zinapigania ubingwa huwa hazifanyi makosa kabisa kwenye kutumia muda kama huu wa usajili kusajili wachezaji ili kuimarisha kikosi kwa ajili ya kuwania ubingwa lakini shida inakuja kwa timu ambazo zipo zipo tu, hizi huwa hazitumii muda huu kusajili bali hadi dirisha likifungwa ndio zinapozinduka na kuanza kuilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwa limeweka muda mdogo wa usajili.
Kundi hili ndilo lililomaliza mzunguko wa kwanza likiwa limetanguliza mguu mmoja chini ya daraja la kwanza, kwani alamu nyekundu ya hatari ilishalia, kwa hiyo zitahitaji kushindana kwa nguvu zote kusaka ushindi ili kujinasua kwenye hatari hiyo.
Ukiangalia msimamo wa ligi kuu mpaka sasa wakati tunasubiri mzunguko wa pili, timu za kundi la kwanza unaweza kusema ni vinara Simba, Yanga, Azam pamoja na Kagera Sugar. Wakati kundi la mwisho ni Toto African, Mwadui na JKT Ruvu zinazopumulia mashine wakati Mbao, Maji Maji na African Lyon zitatakiwa kupambana ili kujiepusha kwenye kitanzi hicho.
Nina fikiria kuwa makocha wa timu zote 16 wameona mapungufu ya vikosi vyao na wapi walipokosea na ni aina gani ya wachezaji wanaowahitaji ili kuimarisha vikosi vyao katika kuleta ushindani kwenye ligi mzunguko wa pili iliyopangwa kuanza Desemba 17 na ndio inayotoa taswira ya bingwa msimu wa ligi 2016/2017.
Nina hisi kuwa viongozi na benchi la ufundi la timu hizo watatumia vema dirisha hili dogo la usajili ambalo litafunguliwa Novemba 15, kwa ajili ya kuboresha timu zao, ili kuongeza ushindani kwenye mzunguko wa pili wa ligi ambao ndio hasa utatoa picha ya ubingwa kwa msimu huu.
Mpaka kufikia sasa makocha wameshajua nini cha kufanya katika kuboresha vikosi vyao kwa kujua nani wa kumuongeza na yupi wa kumuacha kwenye kikosi.
Nafikiria kuwa viongozi wa timu waachie mabenchi yao ya ufundi, kufanya usajili wa kina, ili kuunda vikosi vilivyo imara na sio viongozi kupiga siasa kwa kuacha wachezaji kwa sababu ya kutokuwa na maelewano mazuri na mchezaji huyo au unataka kumleta mchezaji ambaye utapata asilimia fulani ya mshahara wake.
Aidha, nafikiria kuwa Makocha wapewe uhuru ili wasajili wachezaji bora kutokana na uwezo na mahitaji yao, huku wale wanaoachwa basi nao waachwe kistaarabu na kupatiwa stahiki zao kuepusha malumbano yasiyo na tija.
Naamini kuwa wadau na mashabiki wanahitaji kuona ligi kuu Tanzania bara ikiwa ya ushindani wa hali ya juu, ili jambo hilo lionekane ni lazima kuwe na usajili mzuri kwenye timu 16 zinazochuana kwenye Ligi Kuu Bara.
Usajili mzuri kwa kila timu utaifanya ligi yetu kuwa moja ya ligi bora katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, pia utazifanya timu zetu kufanya vema kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
'Ikiwa usajili wa kuboresha vikosi ukifanyika vema basi mzunguko wa pili utakuwa na ushindani zaidi ya wa kwanza uliofikia tamati Alhamisi iliyopita'.
EmoticonEmoticon