Millionaire  Ads

Sunday, November 13, 2016

habari za michezo

Tags

Penina kidedea Muungano

NA MWANDISHI WETU

MCHEZAJI wa timu ya netiboli ya Jeshi Stars, Penina Mayunga amekuwa mchezaji bora wa michuano ya netiboli kombe la Muungano iliyomalizika juzi jioni viwanja vya Sigara Dar es Salaam.
Michuano hiyo iliyoshirikisha timu nne kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ilikuwa na msisimko mkubwa na timu ya Uhamiaji kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Uhamiaji ilitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga Polisi Morogoro kwa jumla ya mabao 44-35 katika mchezo wa fainali ulioonekana kuwa mkali na ushindani.
Akizungumza Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) Anna Kibira alisema baada ya fainali hiyo kamati ya ufundi ya michuano hiyo ilikaa na kuchambua wachezaji waliofanya vema  tangu michuano hiyo ianze na kuona Penina alistahili kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo.
Alisema licha ya timu yake kutocheza fainali, mchezaji huyo alionesha nidhamu ya mchezo kuanzia mchezo wa kwanza hadi hatua ya nusu fainali hatua iliyowavutia viongozi na hata kamati ya mashindano hayo.
"Baada ya michuano kumalizika kamati ya ufundi ilitoa orodha ya wachezaji ambao wamefanya vema tangu michuano ya kombe la muungano ianze ambapo Penina ndeye mchezaji aliyeonekana kuwazidi wachezaji wenzake kwa kuongoza kufanya vema ikiwemo nidhamu ndaangu mwanzo hadi mwisho wa michuano,"alisema Kibira.
Alisema michuano hiyo imekuwa ikiwaunganisha pamoja na kudumisha uhusiano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar hali inayosababisha kufanya michuano hiyo kila mwaka kwa mfumo wa kupokezana.
"Mwakani michuano hii itafanyika Zanzibar na timu za Tanzania Bara zitapata fursa ya kusafiri kuwafuata wenzetu hivyo tunamshukuru mungu kwa mwaka huu kuweza kutusaidia kumaliza salama michuano hii,"alisema Kibira.
Alisema bingwa wa michuano hiyo anabaki kuwa bingwa lakini hakuna nafasi ya kuwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa isipokuwa bingwa wa michuano ya klabu bingwa Tanzania ndiye anayepata nafasi ya kucheza michuano ya Afrika Mashariki ambapo timu hiyo hiyo ya Uhamiaji ndiyo iliyotwaa pia kikombe cha ubingwa wa klabu bingwa Tanzania michuano iliyofanyika mapema mwaka huu mjini Dodoma.

Mwisho
@@@@@@@@

Yanga kutimkia Ulaya

NA MWANDISHI WETU
UONGOZI wa Yanga upo kwenye mipango ya mwisho kuipeleka timu hiyo kupiga kambi barani Ulaya ili iweze kujipanga vema kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Yanga imemaliza mzunguko kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 32 nyuma ya vinara wa timu hiyo Simba ambayo ina pointi 35 baada ya mechi 15 kwa kila mmoja.
Yanga imefikisha pointi hizo baada ya kushinda michezo 11, ikifungwa michezo miwili  na kutoka sare michezo miwili .
Yanga mwakani itacheza michuano ya klabu Bingwa Afrika, huku Azam ikiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika michuano ya klabu bingwa kwa mwaka huu, Yanga ilishia hatua ya 16 bora , na kufanikiwa kutinga hatua ya Makundi ya kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilimaliza katika kundi A ikiwa nafasi ya nne kwenye kundi lililokuwa na timu Kama TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mo Bejaia ya Algeria na Madeama ya Ghana.
Akizungumza Dar es Salaam jana, mmoja wa viongozi wa Yanga, alisema mipango iliyopo sasa ni kutafuta kambi tulivu kwa timu yao ambayo wamepanga iende barani Ulaya.
Alisema wanatambua changamoto na ushindani mkubwa uliopo kwenye ligi msimu huu lakini pia ugumu wa michuano ya kimataifa hivyo wanataka kujiimarisha kabla ya muda kufika.
"Tupo kwenye mipango ya kuona kambi itawekwa nchi gani , lakini hasa hasa barani Ulaya, baada ya mipango kukamilika tutawafahamisa itakuwa ni nchi gani,"alisema kiongozi huyo.
Yanga inadaiwa itapiga kambi nje ya nchi ikiwa na benchi jipya la ufundi chini ya  kocha Mzambia George Lwandamina atakayekuwa akisaidiwa na Charles Boniface Mkwasa na Manyika Peter kocha wa makipa.
Kocha huyo atatua na baadhi ya nyota wake  wa kigeni ambapo baadhi ya wachezaji wa kigeni waliopo sasa wapo watakaoachwa na wengine kutolewa kwa mkopo.
Hata hivyo  hadi sasa Yanga bado haijaweka wazi juu ya maamuzi hayo ya kulitengua benchi lote la ufundi kutokana na kutokuwa na msemaji wa moja kwa moja kulizungumzia suala hilo.
Lakini habari za uhakika ni kwamba tayari  Lwandamina amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo kuanzia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

@@@@@@@

Yoso 17 wapeta Azam


NA ABDUL DUNIA


VIJANA saba wenye umri chini ya miaka 17, wamepenya kwenye majaribio ya wazi ya mwisho katika mkoa wa Dar es Salaam, yaliyoendeshwa na Klabu Azam
Huo ni mwendelezo wa mpango wa kutengeneza timu bora ya vijana wa umri huo kwa ajili ya kuwatumia kwa miaka ijayo na wengine kunufaika nao kwa kuwauza.
Katika majaribio hayo yaliyofanyika juzi uwanja wa Azam Complex Chamazi Dar es Salaam, vijana 433 wenye umri tofauti kuanzia chini ya umri wa miaka 10, 12, 14 na 17 walijitokeza, ambapo waliweza kuchaguliwa saba na wengine 33 kuorodheshwa.
Mpaka sasa mpango huo umeshahusisha mikoa mitano ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Dodoma na Visiwani Zanzibar, ambako kote kumefanya idadi ya vijana waliofanyiwa usaili kufikia 2,593, kati ya hao 50 pekee ndio waliochaguliwa kushiriki fainali ya mwisho itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex mwezi ujao.
Mbali na hao 50, wengine 96 wameorodheshwa na kuhifadhiwa kama akiba ya baadaye.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, alisema kuwa amefurashishwa na vijana waliojitokeza kwenye majaribio hayo huku akidai kuwa viwango vilikuwa ni vya hali ya juu.
"Wamejitokeza vijana wadogo sana wanaotoka maeneo ya Chamazi na Mbagala, nimefurahishwa sana kuwaona viwango vilikuwa juu na kiukweli ilikuwa nji nzuri ya kumaliza majaribio Dar es Salaam," alisema.
Alisema kuwa mara baada ya kumaliza vema zoezi hilo Dar es Salaam, hivi sasa mipango iliyopo ni kuthibitisha tarehe za majaribio mengine ya wazi kwenye maeneo yaliyobakia Tanzania.
"Kwa sasa tunachoangalia ni kwenda kwenye maeneo mengine manne kwenye mikoa ya Mbeya, Kigoma, Mwanza na tutahudhuria michuanio ya vijana Arusha Desemba mwaka huu, baada ya hapo katikati ya mwezi Desemba tutafanya fainali ya mwisho hapa Chamazi, ambayo itatoa majibu ya timu yetu ya vijana chini ya umri wa miaka 17," alisema.


EmoticonEmoticon